1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Silaha nzito zinatumika katika mapigano Darfur: UN

Bruce Amani
12 Mei 2024

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti kwamba silaha nzito zinatumika katika mapigano katika mji wa El-Fasher nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4fl0D
Eneo la soko la mifugo lililoteketezwa mjini El-Fasher
Mji wa El-Fasher umeshuhudia mapigano makali kati ya vikosi vya Sudan na wanamgambo wa RSFPicha: AFP

Katika taarifa, Nkweta-Salami amesema kuwa raia waliojeruhiwa wanakimbizwa hospitali huku wengine wakijaribu kukimbia mapigano katika eneo hilo la Darfur.

Mjumbe huyo amesema kuwa ana wasiwasi mkubwa juu ya kuzuka kwa mapigano hayo huko El-Fasher licha ya wito wa mara kwa mara kwa wahusika katika mzozo huo kuacha kushambulia mji huo.

Hospitali ya MSF mjini El Fasher
Mapigano ya El-Fasher yanatishia maisha ya zaidi ya raia 800,000 wanaoishi mjini humoPicha: ALI SHUKUR/AFP

Nkweta-Salami alisisitiza kuwa ghasia hizo zinatishia maisha ya zaidi ya raia 800,000 wanaoishi mjini humo.

"Nina wasiwasi pia na ripoti za matumizi ya silaha nzito na mashambulizi katika maeneo yenye watu wengi katikati ya mji wa El Fasher na viunga vyake, na kusababisha vifo na majeruhi." Aliongeza.

Soma pia: Mataifa ya Ulaya yafanya kongamano kuichangia fedha Sudan

Mwezi Aprili, Marekani ilionya kuhusu hatari ya mashambulizi ya waasi wa kijeshi mjini humo, ambao ni kitovu cha misaada ya kibinadamu kinachoonekana kuwa kitovu cha mzozo mpya wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mwaka mmoja wa vita vya Sudan

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, Sudan imekumbwa na vita kati ya jeshi, linaloongozwa kimsingi na kiongozi wa nchi hiyo Abdel Fattah al-Burhan, na vikosi vya wanamgambo wa RSF, vinavyoongozwa na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo. Vita hivyo vimewauwa makumi kwa maelfu ya watu na kuwalazimu zaidi ya milioni 8.5 kuyakimbia makazi yao katika kile Umoja wa Mataifa unaita "mgogoro mkubwa zaidi duniani wa watu kuyakimbia makazi yao."

El Fasher ndio mji wa mwisho mkubwa katika jimbo la Darfur ambao hauko chini ya udhibiti wa RSF na Marekani ilionya mwezi Aprili kuhusu kitisho cha kufanyika mashambulizi mjini humoKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Jumamosi kuwa ana "wasiwasi mkubwa kuhusu vinavyoendelea Sudan." Amesema panahitajika usitishwaji haraka wa mapigano na juhudi zilizoratibiwa za kimataifa za kuongoza mchakato wa kisiasa unaoweza kuirejesha nchi hiyo kwenye mkondo sahihi.

afp