1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina na kumbukumbu ya miaka 76 ya Nakba

Amina Mjahid
15 Mei 2024

Kumbukumbu hiyo iitwayo Nakba inafanyika wakati Wapalestina wakiendeleza harakati zao za kupigania uhuru wao, hali inayosababisha migogoro ya mara kwa mara.

https://p.dw.com/p/4frtp
Wapalestina mwaka 1948
Wapalestina wakikimbia ardhi yao mwaka 1948Picha: ELDAN DAVID/EPA/dpa/picture-alliance

Nakba, neno la Kiarabu linalomaanisha janga, ndilo lililotumika kuelezea masaibu ya Wapalestina kufurushwa kwa nguvu katika makaazi yao. Wapalestina 700,000 walifurushwa majumbani mwao wakati wa vita vya Israel na Waarabu mwaka 1948, vilivyofungua njia ya kuundwa rasmi dola la Israel.

Baada ya vita hivyo, Israel ilikataa Wapalestina kurejea makwao, kwasababu hatua hiyo ingesababisha Wapalestina kuwa wengi- katika mipaka ya eneo hilo.

Soma: Nakba - "maafa" ya Wapalestina

Badala yake wakageuka kuwa wakimbizi wa kudumu ambao kwa sasa idadi yao imeongezeka na kufikia milioni 6 huku wengi wakiishi katika maeneo duni kama makambi ya wakimbizi yalioko Lebanon, Syria, Jordan na katika eneo lililozingirwa na wanajeshi wa Israeli la Ukingo wa Magharibi.

Katika Ukanda wa Gaza, wakimbizi hao wanachangia robo tatu ya idadi hiyo ya watu.

Wapalestina mwaka 1948
Wapalestina wakikimbia ardhi yao mwaka 1948Picha: ELDAN DAVID/EPA/dpa/picture-alliance

Kukataa kwa Israel, kwa kile Palestina inachosema ni haki yao ya kurejea katika ardhi yao, kumekuwa jambo linaloendelea kuzua mvutano katika mzozo wa Mashariki ya Kati, na ndilo jambo lililoweka kizingiti katika mazungumzo ya upatikanaji amani yaliyokwama miaka 15 iliyopita. Kwa sasa Wapalestina wanahofu kubwa ya kurejea kwa janga la Nakba, lililoandika historia  ya uchungu.

Fuatilia: Wapalestina kesho, wataadhimisha ya miaka 76 kuondoshwa katika ardhi yao.

Kote mjini Gaza katika siku za hivi karibuni Wapalestina wamekuwa wakipakia mizigo yao kwenye magari pamoja na mikokoteni inayoendeshwa na punda na wengine hata kwenda kwa mguu, katika eneo ambalo tayari limejaa watu la Rafah, wakati Israel ikiendelea kutanua operesheni zake za kijeshi mjini Gaza.  Picha zinazoonekana katika mzozo huu mpya wa Mashariki ya kati uliodumu kwa miezi saba sasa, zinafanana kabisa na picha zilizochukuliwa zaidi ya miaka 70 iliyopita katika janga la Nakba.

Wapalestina wanahofia kurejea kwa janga la Nakba

Mustafa al-Gazzar, aliye na miaka 81 hadi sasa anakumbuka namna walivyofurushwa majumbani mwao katika eneo ambalo sasa linajulikana kama Israel ya Kati ikiwa kusini mwa mji wa Rafah. Gazzar anasema alikuwa na miaka mitano kisa hicho kilipotokea. Ameongeza kuwa  ipo siku waliposhambuliwa kutoka angani na wakati mwengine walichimba mahandaki kujilinda na pia kujikinga na baridi.

Al-Gazzar, ambae sasa ni Babu aliye na wajukuu na vitukuu, amelazimika kukimbia tena, na safari hii kupelekwa katika kambi ya Muwasi kunakoishi Wapalestina takriban 450,000. Anasema hali ilivyo sasa ni mbaya zaidi kuliko ile iliyoonekana mwaka 1948, ambako shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi wa Palestina lilikuwa linauwezo wa kutoa chakula na mahitaji mengine muhimu kwa wakimbizi hao.

"Matumaini yangu mwaka 1948 yalikuwa kurejea katika ardhi yangu lakini matumaini yangu sasa ni kuishi, naishi kwa uoga siwezi hata kuwatafutia wanangu na wajukuu zangu," alisema Gazzar huku akibubujikwa na machozi. Vita vya Gaza vilisababishwa na hatua ya wanamgambo wa Hamas kuvamia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 na kusababisha mauaji ya watu 1,200 huku wengine wakichukuliwa mateka.

Hali ya kibinadamu: Zaidi ya watu 500,000 wakimbia mapigano Rafah, UN

Baadae Israel ikaanza mashambulizi ya kulipiza kisasi yanayoendelea hadi sasa ambapo wapalestina zaidi ya 34,000 wameuwawa wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Vita hivyo pia vimewakosesha makaazi Wapalestina milioni 1.7. na hiyo ni mara mbili ya idadi ya watu waliotoroka kabla na baada ya janga la Nakba.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

Hata kama Wapalestina hawajaondolewa kwa nguvu na kwa wingi kutoka katika ukanda wa Gaza, wengi wanahofia kwamba hawatoweza kurejea nyumbani  au uharibifu uliosababishwa na mamkombora ya Israel yaliyovurumishwa katika eneo hilo yatafanya iwe vigumu kuendelea kuishi huko.Mapigano makali yautikisa Ukanda wa Gaza ikiwemo mji wa Rafah

Tathimini  ya hivi karibuni iliyofanywa na Umoja wa Mtaifa imeonyesha itachukua muda hadi mwaka 2040 kujenga upya nyumba zilizoharibiwa.